Vyama vya upinzani nchini Chad vyasusia uchaguzi wa bunge na madiwani

Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno akishukuru umati wa watu walioshiriki kampeni ya mwisho ya uchaguzi wa rais mjini N'Djamena, Mei 4, 2024. Picha ya AFP

Chad imefanya uchaguzi mkuu Jumapili unaoelezewa na serikali kama hatua muhimu kuelekea kumaliza utawala wa kijeshi, lakini uchaguzi huo umesusiwa na vyama vya upinzani.

Watu wachache walijitokeza kupiga kura katika mji mkuu N’Djamena wakati vituo vya kupigia kura vilipofunguliwa kwa wapiga kura kuchagua bunge jipya, mabunge ya majimbo na madiwani.

Maafisa wa uchaguzi katika wilaya ambako familia ya rais na viongozi wakuu wanaishi wamesema wapiga kura hawakujitokeza kwa wingi kutokana na “ hali ya baridi”.

Vyama vya upinzani vilikuwa vimewasihi wapiga kura milioni 8 kususia uchaguzi, vikidai kuwa matokeo yake tayari yanajulikana.

Kususia huko kunaacha uwanja wazi wa ushindi kwa wagombea wanaomuunga mkono Rais Mahamat Idriss Deby Itno, ambaye aliingizwa madarakani na jeshi mwaka 2021 na kuwa kiongozi halali katika uchaguzi wa rais mwezi Mei ambao wagombea wa upinzani walisema uligubikwa na wizi.