Vita Sudan vyawakutanisha wasomi wa jadi na vikosi vya vijijini vilivyotengwa

Wakimbizi wa Sudan wakiomba hifadhi nchini Chad.

Vita vya kikatili vya Sudan vimewakutanisha wasomi wa jadi wa mijini ambao kwa muda mrefu wameshikilia mali na mamlaka katika mji mkuu wa Khartoum dhidi ya vikosi vingine vya  vijiji vilivyotengwa, wachambuzi wanasema.

Kwa zaidi ya mwezi uliopita, majenerali wawili mahasimu wanapigania udhibiti katika taifa hilo la kaskazinimashariki mwa Afrika katika mapigano ambayo yameeneza vurugu, na kusababisha vifo vya karibu watu elfu moja na kuwakosesha makazi karibu milioni moja.

Mmoja wao ni mkuu wa jeshi Abdel Fattah al Burhan, mwanajeshi wa siku nyingi, mzaliwa wa kaskazini mwa khartoum ambaye alimpindua kiongozi wa kiislamu wa muda mrefu Omar al-Bashir baada ya maandamanano makubwa na kisha kuchukua madaraka kamili mwaka 2021.

Mwingine ni makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo ambaye aliwahi kuwa mfugaji ngamia kutoka mkoa wa magharibi wa Darfur unaopakana na Chad ambaye sasa anaongoza kundi la RSF.