Vikwazo vipya Marekani kulenga Tanzania, China, Korea Kaskazini

Steven Mnuchin akisubiri kuhutubia kabla ya kuanza kutoa maelezo juu ya vikwazo vipya ikulu ya White House huko Washington, Feb. 23, 2018.

Steven Mnuchin akisubiri kuhutubia kabla ya kuanza kutoa maelezo juu ya vikwazo vipya ikulu ya White House huko Washington, Feb. 23, 2018.

Baada ya Marekani kutangaza kuwa itaiwekea Korea Kaskazini vikwazo vikali zaidi katika mitandao yake ya kibiashara duniani kote, Ijumaa Rais Donald Trump alitishia kuwepo “awamu ya pili” ya vikwazo iwapo vya kwanza vinalegalega.

“Kama vikwazo hivyo havina athari, itabidi twende kwenye awamu ya pili, na hivi vya awamu ya pili vitakuwa ni kitu kibaya sana,” Trump amesema, wakati akizungumza akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Australia Malcolm Turnbull ikulu ya White House ambaye anazuru Marekani.

Hata hivyo Trump hakufafanua alimaanisha nini kwa kusema “awamu ya pili” lakini alikuwa akionya kuwa itakuwa ni hali ya kusikitisha sana kwa dunia,” akiongeza kuwa: “Tusubiri tutaliona hilo.”

Vikwazo hivyo vitalenga makampuni 56- mashirika ya meli 27 na biashara, meli 28 na mtu mmoja- duniani kote , kutoka Korea Kaskazini mpaka China, hadi Tanzania kwa mujibu wa maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani.

https://www.voaswahili.com/a/tanzania-yakiri-mahusiano-yake-na-korea-kaskazini/4030550.html

Wakati huo huo Waziri wa Fedha Marekani ametoa onyo Ijumaa kwa mataifa yanayoshirikiana kibiashara na Korea Kaskazini kwamba yanafanya hivyo kwa kujiweka katika nafasi mbaya sana.

Akitangaza vikwazo vipya Waziri Steve Mnuchin amesema kuwa kampuni yoyote duniani iliyosaidia kufadhili mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini itapoteza haki ya kufanya biashara na Marekani.

Pia aliwaambia waandishi kwamba Marekani sasa huenda ikaanza kusimamisha na kupekua meli zinazo safirisha mizigo Korea Kaskazini.

Rais wa Marekani Donald Trump Ijumaa aliviita vikwazo hivyo vikali zaidi, lakini duru za habari duniani zinasema kuwa tayari vikwazo kama hivyo vilishawekwa hapo awali na kulenga mitandao mbalimbali ya kibiashara ya Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini tayari inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa pamoja na vile vya Marekani kuhusu mpango wake wa Kinyuklia.

Hata hivyo taifa hilo limeendelea kukaidi na kuendeleza programu yake ya nyuklia na makombora ya masafa ya mbali.

Mwaka 2017 ilifanya majaribio ya silaha za kinyuklia mbali na mkombora ya masafa marefu yanayoweza kufika Marekani.

Marekani imeeleza kuwa vikwazo vipya vinalengo la kuidhibiti zaidi Korea Kaskazini, kwa njia ya kukata vyanzo vyake vya fedha na nishati ili kukomeshaprogramu yake ya nyuklia.