Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 12:27

Tanzania yakiri mahusiano yake na Korea Kaskazini


Waziri Mahiga
Waziri Mahiga

Tanzania imetoa ufafanuzi juu ya mahusiano yake na Korea Kaskazini na kuwa tayari ilikuwa imekwisha tengeneza utaratibu wa kuweza kusitisha mahusiano hayo.

Akizungumza na waadishi wa habari Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dr Augustine Mahiga amesema kuwa Tanzania ilikuwa tayari imekubali kutekeleza agizo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kusitisha mahusiano hayo.

Waziri huyo ameeleza kuwa Tanzania haina ugomvi wowote na Korea Kaskazini lakini kitendo chao cha kutengeneza silaha za maangamizi hakikubaliki.

“Lakini kitendo chao cha kutengeneza silaha za kuangamiza sio kizuri,” alieleza.

Dr Mahiga amesema kuwa kwa heshima ya ustaarabu duniani na usalama duniani ndio maana tukaanza kuchukua hatua za kupunguza mahusiano na kuhakikisha vile vikwazo vinaanza kuwabana.

“Kama ni meli, kama ni misaada ya karibu tukapunguza punguza,” amefafanua waziri.

Lakini amesema kuwa maamuzi yakitolewa na Baraza la Usalama wanategemea kwamba tuyatekeleze katika kipindi cha masaa 24.

“Haya jamani mie nakubali lakini hata hivyo sisi tulifanya uungwana tukasema tutatengeneza utaratibu wa kuweza kuondoa hayo mahusiano,” amesema Waziri Mahiga.

Pia Dr Mahiga amekiri kuwa Tanzania ilikuwa na uhusiano na Korea Kaskazini kibiashara.

please wait

No media source currently available

0:00 0:00:59 0:00

“Tulikuwa na uhusiano wa kibiashara na makampuni na sio serikali ya Korea Kaskazini kusaidia vitu fulani ambavyo tunahitaji kwa ajili ya ulinzi na usalama wa jeshi letu,” Waziri Mahiga amesisitiza.

Ripoti ya Septemba 9 ilitolewa siku mbili kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa pamoja kuweka vikwazo vipya vinavyo ishinikiza Korea Kaskazini kufanya mazungumzo juu ya silaha zake za nyuklia.

Jopo la watu wanane limesema linafanya tathmini juu ya taarifa kutoka kwa vyanzo vya habari vya nchi wanachama wa UN ambavyo havijatajwa majina vikisema kuwa Tanzania iliingia mikataba ya kijeshi na Korea Kaskazini yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 12.5.

Kampuni ya Haegeumgang Trading Corporation inasemekana kuwa inafanya ukarabati na kurekebisha mifumo ya makombora ya kivita na ulinzi wa anga kuifanya iwe ya kisasa.

Jopo hilo limeongeza kuwa limeendelea kufanya uchunguzi wake juu ya Korea Kaskazini kutoa mafunzo ya kijeshi kwa jeshi la Uganda na vikosi vya polisi nchini humo, “hususan Jeshi la Anga la Uganda.”

Pia uchunguzi huo umejikita katika shughuli zinazofanywa na mwakilishi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Korea Mining Development Trading Corporation ambaye alisafiri kwenda Uganda akitokea Syria.

Pia jopo hilo limeongeza kusema kuwa linafuatilia kazi ya mwambata wa kijeshi katika ofisi ya ubalozi wa Korea Kaskazini nchini Kampala.

“Uganda bado haijajibu maswali yaliyoulizwa na jopo hilo,” ripoti hiyo imesema.

XS
SM
MD
LG