Nuland, afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani, akutana na watawala wa kijeshi wa Niger

Senate US Ukraine Russia

Afisa mmoja mwandamizi, wa serikali ya Marekani, amezuru Niger kuwahimiza watawala wapya wa kijeshi, kumrejesha madarakani rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

Waziri mdogo wa wizara ya mambo ya nje anayehusika na masuala ya siasa, Victoria Nuland, alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X, uliojulikana awali kama Twitter, kwamba alisafiri hadi mji mkuu wa Niamey ili "kuelezea wasiwasi wake juu jaribibio linalokiuka maadili ya kidemokrasia, la kunyakua mamlaka, na akahimiza umuhimu wa kurejelea utaratibu wa kikatiba."

Nuland aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba alikutana na mtu "aliyejitangaza kuwa mkuu wa ulinzi" Brigedia Jenerali Moussa Salaou Barmou, na maafisa wengine watatu wa kijeshi wakati wa ziara yake, akielezea mazungumzo hayo kuwa "ya wazi kabisa, na wakati mwingine, magumu sana."

Alisema maafisa wa kijeshi "wako imara kabisa kuhusu jinsi wanataka kuendelea," njia ambayo anasema "haiendani na katiba ya Niger." Amesema viongozi wa mapinduzi walikataa ombi lake la kukutana moja kwa moja na Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum na familia yake, pamoja na kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdourahamane Tchiani.

Nuland, ambaye pia ni kaimu naibu waziri wa mambo ya nje wa sasa, anasema aliombwa na Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken kusafiri hadi Niamey "kuona kama masuala hayo yanaweza kutatuliwa kidiplomasia" na kuweka wazi kwa uongozi wa kijeshi, kwamba Washington inaweza kusitisha ushirikiamno wa kiuchumi, na aina nyingine za msaada kwa Niger "kama demokrasia haitarejeshwa."

Nchi za Afrika Magharibi, na mataifa yenye nguvu duniani yanatumai kwamba bado kuna fursa ya upatanishi, kati ya viongozi wa mapinduzi ya Niger na wale walioongoza nchi hiyo kidemokrasia, kabla ya mkutano wa kilele wa Alhamisi, ambao huenda ukakubaliana, juu ya uingiliaji wa kijeshi, na kurejesha demokrasia katika nchi hiyo.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imepanga mkutano huo, ili kujadili mvutano wake na serikali ya kijeshi ya Niger, ambayo ilichukua mamlaka mnamo Julai 26, na kupuuza masharti yaliyowekwa, ya kurejesha utawala wa kidemokrasia kufikia Jumapili Agosti 6.

Viongozi hao wa mapinduzi wameapa kupinga shinikizo kutoka nje,za kutaka kumrejesha madarakani rais aliyeondolewa, Mohamed Bazoum, baada ya ECOWAS kuwawekea vikwazo, na washirika wa Magharibi kusitisha msaada.

Mapinduzi hayo ya saba ya kijeshi katika ukanda Afrika Magharibi na Kati katika kipindi cha miaka mitatu, yamevutia hisia za kimataifa, kwa kiasi fulani kutokana na nafasi muhimu ya Niger, katika vita na wapiganaji wa Kiislamu, na hifadhi yake ya madini ya uranium na mafuta, ambayo inaipa umuhimu wa kiuchumi na kimkakati kwa Marekani, Ulaya, China, na Russia.

"Hakuna shaka kwamba diplomasia ndiyo njia bora ya kutatua hali hii," Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliambia kituo cha redio cha Ufaransa RFI siku ya Jumanne.

Marekani inaunga mkono juhudi za jumuiya ya kikanda kurejesha utulivu wa kikatiba, alisema. Hata hivyo, hakutoa maoni yake kuhusu mustakabali wa wanajeshi 1,100 wa Marekani, walio nchini Niger.