Utawala wa kijeshi nchini Niger wasitisha matangazo ya BBC

Kiongozi wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahamane Tiani

Niger Alhamisi ilitangaza kwamba imesitisha matangazo ya radio BBC kwa miezi mitatu, huku shirika hilo la utangazaji la Uingereza likiingia kwenye orodha ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vilivyoadhibiwa na serikali za kijeshi katika kanda ya Sahel.

Marufuku ya BBC inadaiwa inahusu kupeperusha “taarifa potofu zinazoweza kuvuruga amani ya kijamii na kudhoofisha ari ya wanajeshi” wanaopigana na wanajihadi, itaanza kutekelezwa “mara moja” nchini kote, uongozi ulisema.

Vipindi vya BBC vinavyosikilizwa na watu wengi vikiwemo vya lugha ya Kihausa vinapeperushwa nchini Niger kupitia radio washirika nchini humo.

Tangu kukamata madaraka mwezi Julai mwaka 2023 katika mapinduzi, serikali ya kijeshi imepiga marufuku vyombo kadhaa vya habari vya mataifa ya Magharibi.

Kando na BBC, mashirika mawili ya utangazaji ya Ufaransa, Radio France Internationale (RFI) na France 24, yamepigwa marufuku nchini Niger tangu mwezi Agosti 2023.

Alhamisi jioni, utawala wa kijeshi ulisema pia kwamba “umewasilisha malalamiko” dhidi ya RFI.