Waandamanaji wanaomba kiongozi wa chama cha wafanyakazi anayezuiliwa aachiliwe na kupunguza pia bei ya chakula, kukomesha udhibiti wa vyombo vya habari na kuboresha hali ya maisha kwa wafanyakazi wa serikali.
Mgomo huo uliitishwa katika hali ya ongezeko la mvutano wa kijamii na kutokuwepo kwa serikali ya mpito baada ya utawala wa kijeshi kutangaza kuvunjwa kwa serikali wiki iliyopita, bila kueleza sababu.
Katika hotuba kwenye televisheni ya taifa Jumanne jioni, msemaji wa kiongozi wa utawala wa kijeshi Jenerali Mamady Doumbouya alisema “ Bwana Amadou Oury Bah, mchumi, anateuliwa kuwa waziri mkuu na kiongozi wa serikali.”
Msemaji huyo alisema jukumu kubwa la Oury Bah itakuwa kupunguza mvutano na vyama 13 vya wafanyakazi ambavyo viliitisha mgomo ulioanza siku ya Jumatatu, ambao ulisababisha vifo vya watu wawili waliopigwa risasi wakati wa vurugu katika vitongoji vya mji wa Conakry.
Shule, maduka, masoko na barabara zilikuwa tena tupu Jumanne na hospitali zilitoa tu huduma za dharura.