Wizara ya Mambo ya Nje ya Rashia imesema katika tamko lake kuwa pia imeamrisha kufungwa kwa kituo cha utamaduni cha Uingereza nchini Rashia na kusitisha mkataba wa kufungua tena ubalozi mdogo wa Uingereza huko mji wa St. Petersburg.
Tayari imewaamrisha wanadiplomasia hao wa Uingereza kuondoka nchini Urusi katika kipindi cha wiki moja.
Wizara hiyo pia imemwita Balozi wa Uingereza nchini Rashia siku ya Jumamosi kabla ya kutangaza hatua hizo.
Tamko la Wizara hiyo limesema kuwa serikali ya Urusi inaweza kuchukua hatua zaidi iwapo Uingereza itaonyesha vitendo vyovyote “visivyo vya kirafiki” dhidi ya Urusi.
Hivi karibuni Uingereza iliwafukuza wanadiplomasia 23 wa Rashia baada ya Moscow kukataa kutoa maelezo vipi aina ya sumu iliyokuwa ikitumika wakati wa utawala wa Soviet iliweza kutumika katika mji wa Salisbury- Uingereza kumshambulia jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal na binti yake, Yulia.
Kulipiza kisasi kuliko tangazwa na Waziri Mkuu Theresa May katika Bunge la Uingereza kumepelekea kuanza kwa vita ya kiuchumi dhidi ya Rais wa Rashia Vladimir Putin na kikundi cha watu wachache wenye maslahi ya pamoja cha maafisa wa serikali ya Kremlin na wafanyabiashara matajiri wenye ushawishi wa kisiasa.
Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia rasilmali zao ambazo wanazimiliki Uingereza pamoja na kunyimwa viza kwa watu binafsi wote waliotajwa katika sakata hilo.
Waziri Mkuu anawashinikiza washirika wa kimataifa kufuata hatua iliyochukuliwa na Uingereza na kuanza kuangaza mabilioni ya dola ambazo Kremlin imewekeza katika rasilimali zake ulimwenguni kote.