Kiongozi huyo amesema kuwa kumekuwa na athari za Serikali kuvunja mikataba ya wawekezaji wa nje kwani wanasheria wanaoishauri serikali wamekuwa hawatekelezi wajibu wao inawezekana ni kwa sababu ya kuogopa kutumbuliwa.
Lissu ambaye ni mwanasheria Mkuu wa Chadema alidai Ijumaa kuwa utekelezaji wa ununuzi wa ndege ya tatu kutoka kampuni ya Bombadier ya nchini Canada umezuiliwa nchini Canada na kampuni hiyo ya ujenzi kwa kuwa inaidai serikali Dola 38.7 milioni za Marekani (Sh 87 bilioni).
Vyanzo vya habari vinasema kuwa kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.
Lakini kwa upande wake serikali imesisitiza kuwa licha ya deni hilo, ndege hiyo itakuja huku ikiwatuhumu wanasiasa kutengeneza mgogoro huo.
Serikali kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa Jumamosi imesema kwamba hatua za kidiplomasia na za kisheria zinachukuliwa ili kumaliza jambo hilo na ndege hiyo itawasili wakati wowote nchini.
Kaimu Msemaji ameongeza kuwa taarifa ya wanasiasa hao inadai kwamba kuna wanasheria wa kampuni fulani ya nchini Italia wameweka zuio la la ununuzi wa ndege hiyo kwa madai kwamba wanakamata mali hiyo kwa kuwa kuna kampuni inayoidai Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Kawawa, wanasheria waliofungua madai kwamba Serikali inadaiwa na kwamba ndege hiyo ishikiliwe hawana uhalali wowote wa kufanya hivyo na ni matapeli ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wasioitakia mema Tanzania.
“Kwa kuwa Serikali ilishapata fununu kwamba kuna baadhi ya viongozi wa chama cha siasa wana mpango huo, sasa watu hao wamejidhihirisha hadharani kwamba wao ndio wako nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa maslahi yao,” alisema Kawawa na kuongeza: “Serikali ya Awamu ya Tano inawahakikishia Watanzania kwamba ndege itakuja.
Wanaokwamisha jitihada za serikali za kuleta ndege watapanda, na ndugu zao watapanda, na wafuasi wao watapanda pia.” Aliongeza kuwa mbali na kutaka kuhujumu juhudi za ununuzi wa ndege hiyo, kundi hilo la baadhi ya viongozi wa siasa wameshawahi kushawishi wafadhili wasilete misaada tena Tanzania na kuwaomba washirika wa maendeleo pia wasilete misaada nchini.