Umoja wa Ulaya wataka serikali ya Tanzania iwajibike

Rais John Magufuli

Umoja wa Ulaya (EU) umelaani kuongezeka kwa vitendo vya uvunjifu wa amani ukiwalenga wanasiasa na vitisho nchini Tanzania, na kutaka hatua kuchukuliwa mara moja kukomesha hali hiyo.

Tamko lililotolewa Ijumaa, Februari 23, na kusainiwa na kaimu balozi wa EU nchini, Charles Stuart limesema hali hiyo ambayo inahusisha mauaji na kupotea kwa wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu inatia wasiwasi.

“Tumeingiwa na wasiwasi kwa matokeo ya hivi karibuni ambayo yanatishia kuangamiza maadili ya kidemokrasia na haki za Watanzania katika nchi ambayo inaheshimiwa duniani kote kwa utulivu, amani na uhuru wake,” sehemu ya tamko hilo limeeleza.

Kadhalika EU imeongeza kuwa imesikitishwa na kupigwa risasi na kuuwawa kwa mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji Akwilina Akwilini, tukio lililojiri mwisho wa wiki iliyopita, na wanaunga mkono wito wa Rais Magufuli akita uchunguzi ufanyike mara moja.

Pia wametaka hatua zaidi zichukuliwe, EU imesema, ikiwemo uchunguzi wa kina juu ya mauaji ya wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu.

“Tumeingiwa na wasiwasi juu ya kuongezeka kwa ripoti za uvunjifu wa amani katika miezi ya hivi karibuni likiwemo jaribio la kutaka kumuua Mbunge Tundu Lissu na kupotea kwa watu kama mwandishi wa habari Azory Gwanda,” limesema tamko hilo.

“Pia mashambulizi ya utumiaji wa silaha dhidi ya wawakilishi wa serikali, viongozi na raia katika mkoa wa pwani vitendo ambavyo vimetokea kwa miaka miwili sasa.

Umoja wa Ulaya umesema unaungana na watanzania kwa kuitaka serikali kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha amani na usalama wakati wa mchakato wa kidemokrasia (kama vile kupiga kura), Serikali na raia pia kuheshimu sheria.

Tamko hilo limetolewa kwa makubaliano yaliofikiwa na mabalozi wote wa nchi za Umoja wa Ulaya walioko nchini Tanzania na kuungwa mkono na mabalozi wa Canada, Norway na Switzerland.