Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:59

Matukio ya mauaji, kutekwa Tanzania: Waziri, IGP watakiwa kujiuzulu


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mwigulu Nchemba ametakiwa kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji kwa maelezo kuwa ameshindwa kusimamia amani.

Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) na Chama cha ACT-Wazalendo wametoa kauli hiyo Jumapili ikiwa ni siku moja baada ya kupigwa risasi kwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania Mwanafunzi huyo alipigwa risasi akiwa katika daladala wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema.

Kauli ya mtandao huo na chama hicho imetolewa leo baada ya viongozi wao kuzungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa TSNP Taifa, Abdul Nondo amesema endapo Mwigulu hatajiuzulu, wamemuomba Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake.

“Kwa kuwa hivi sasa matukio haya yamekuwa yakishamiri na kushika kasi; watu kutekwa, kupotea, kupigwa risasi na kuuwawa ni muda muafaka sasa kwa Mwigulu kuchukua uamuzi wa kujiondoa katika wizara kuonyesha uwajibikaji,” amesema.

Ameeleza kuwa mnamo mwaka 1977 Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alijiuzulu baada ya polisikutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.

"Tunaamini kwamba huo utakuwa ni mwanzo wa kukaribisha mabadiliko katika Jeshi la Polisi kwani kuondoka kwa mkuu kutawafanya walio chini yake kuondolewa,” amesema.

Nalo gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limeripoti kuwa Mkuu wa Idara ya Sheria TSNP, Deogratias Mahinyila amesema taasisi yao kupitia wanasheria wao na wanasheria mbalimbali watawasaidia walezi na wazazi wa mwanafunzi huyo kufungua kesi ya madai mahakamani, kutokana na uzembe uliofanywa na polisi ili iwe fundisho.

"Tunataka hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya askari polisi waliotenda unyama huu na kukatisha haki ya kusoma na kuishi kwa mwanafunzi mwenzetu kwani wamekiuka sheria na maadili ya kazi yao, katika kulinda amani ya raia," amesema.

Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba awajibike kwa kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu ameshindwa kukomesha mfululizo wa mauaji ya watu wasio na hatia.

Pia, wamewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa nao wajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ikiwamo kulinda usalama wa raia na mali zao.

IGP SIRRO
IGP SIRRO

​Gazeti hilo limesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Licapo Bakari amesema matukio mengi ya mauaji na kupotea kwa watu yanatokea na viongozi hao hawachukui hatua zozote kukomesha hali hiyo.

Amesisitiza kwamba wote wanaouawa na kutoweka katika mazingira tatanishi ni vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa na chachu ya mabadiliko ambayo inatakiwa kulindwa kwa mustakabali wa nchi hii.

Bakari amesema vijana wa ACT Wazalendo wanalaani mauaji ya Akwilina, kwamba tukio la kuuawa kwa binti huyo siyo la kwanza, siku chache zilizopita kiongozi wa Chadema kata ya Hananasifu, Daniel John naye aliuawa na mwili wake kuokotwa kwenye fukwe za Coco.

"Tunataka uchunguzi huru ufanyike kwa kuchunguza matukio yote kuanzia hili la mwanafunzi wa NIT na mengine yote ya mauaji na utekaji," amesema.

XS
SM
MD
LG