Jeshi la Ukraine limekiri kuwa mapigano karibu na mji wa Chasiv Yar yamekuwa “magumu” na “makali” lakini limesisitiza kuwa wanajeshi wake wamesimama imara.
Huku pande zote zikifanya mashambulizi ya anga, Russia ilisema kuwa ndege moja isiyo na rubani ya Ukraine ilishambulia kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho imekikalia tangu muda mfupi baada ya kuanzisha uvamizi wake mwaka 2022.
Ukraine imekuwa ikitoa wito wa dharura kwa Marekani kuanza kuwasilisha muswada wa dola bilioni 60 ambao umekwamishwa na Warepublican katika Baraza la Wawakilishi kwa miezi kadhaa.
“Ni muhimu kuliambia Bunge hasa kwamba ikiwa halitaisidia Ukraine, Ukraine itashindwa vita,” Zelenskiy alisema katika mkutano kwa njia ya video.
Itakuwa vigumu kwa Ukraine kusimama imara bila msaada huo, Zelenskiy aliongeza. “Ikiwa Ukraine itashindwa vita, mataifa mengine yatashambuliwa.”