“Tulipokea tahadhari hiyo kwa uzito, kama tunavyochukulia vidokezo vingine vingi,” ofisi ya uhamiaji na wakimbizi ilisema Jumapili kwenye mtandao wa X kuhusu kidokezo ambacho ilisema ilipokea mwishoni mwa msimu wa joto mwaka jana.
Lakini ofisi hiyo pia imebaini kwamba sio mamlaka ya kufanya uchunguzi na ilitoa taarifa hizo kwa mamlaka husika, kulingana na utaratibu katika kesi kama hizo.
Haikutoa maelezo zaidi kuhusu mshukiwa au aina ya tahadhari.
Polisi katika mji wa Magdeburg, ambako shambulizi lilifanyika Ijumaa jioni, wamesema Jumapili kwamba waliouawa ni wanawake wanne wenye umri ulio kati ya miaka 45, 52, 67 na 75, pamoja na mtoto wa kiume wa miaka 9.
Maafisa walisema watu 200 walijeruhiwa, na 41 miongoni mwao walijeruhiwa vibaya.
Mamlaka zilimtaja mshukiwa kama daktari raia wa Saudi Arabia ambaye aliwasili Ujerumani mwaka 2006 na alikuwa mkazi wa kudumu.
Jumamosi jioni, mshukiwa alifikishwa mbele ya jaji, katika kesi iliyosikilizwa kwa faragha, aliamuru mshukiwa aendelee kukaa ndani kwa kusubiri mashitaka.