Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema kwamba tani 2,000 za chakula zimevuka na kuingia Gaza kwa msaada wa Jordan, na zimesambazwa na Shirika la Mpango wa Chakual Duniani, WFP.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken wiki hii anatarajiwa kufanya mazungumzo nchini Saudi Arabia na Misri, wakati lengo likiwa ni kufanikisha sitisho jipya la mapigano huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa kipalestina, kuongeza juhudi za kimataifa za kufikisha misaada ndani ya Gaza, na kuzungumzia masuala ya utawala, usalama na maendeleo huko Gaza baada ya vita.
Wakati mapigano yakiendelea, maafisa wa Marekani wamerejea kuelezea wasi wasi wao kuhusu mpango wa Israel wa kufanya mashambulizi huko Rafah kwenye mpaka wa Gaza na Misri, ambako zaidi ya wapalestina milioni moja wamechukua hifadhi.