Mpango wa Rwanda ndiyo kitovu cha mkakati wa serikali wa kupunguza uhamiaji na mpango huo unafuatiliwa kwa karibu na nchi nyingine zenye sera inayofanana na hizo.
Mahakama ya Juu ya Uingereza mwezi uliopita ilitoa uamuzi kwamba hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu ambazo ziko katika sheria za ndani za Uingereza.
Mkataba mpya utajumuisha makubaliano kuwa Rwanda haitawafukuza wanaoomba hifadhi na kuwapeleka katika nchi ambmayo maisha au uhuru wao utatishiwa – ni mojawapo ya wasiwasi mkubwa wa mahakama.
Pia kutakuwa na kamati ya ufuatiliaji ili kuwawezesha watu binafsi kuwasilisha malalamiko ya siri kwao moja kwa moja na bodi mpya ya rufaa iliyoundwa na majaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Chini ya mpango uliokubaliwa mwaka jana, Uingereza ilipanga kuwapeleka Rwanda maelfu ya waomba hifadhi ambao walifika katika ufukwe zake bila ya kibali ili kuwazuia wahamiaji wanaovuka kuingina Uingereza kwa kutumia boti ndogo ndogo wakitokea Ulaya.
Kwa upande wa Rwanda imepokea malipo ya awali ya dola milioni 180, na ahadi ya kupewa pesa zaidi kwa ajili ya kufadhili malazi na kuwahudumia wale ambao wamepelekwa huko.
Mkataba mpya unatarajiwa mwishoni mwa wiki hii kufuatiwa na kuchapishwa kwa sheria inayoitangaza Rwanda kwa kuiita nchi salama, mkataba huo uliandaliwa kuzuia changamoto za kisheria dhidi ya mpango wa kuwasafirisha waomba hifadhi
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP