Uganda : Bobi Wine aachiwa kwa dhamana

Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Mgombea urais wa Uganda na muimbaji mashuhuri Bobi Wine ameachiliwa kwa dhamani ijumaa wakati vifo vimefikia 37 vilivyo sababishwa na maandamano makubwa nchini humo.

Mwanasiasa huyo ameachiliwa baada ya maafisa wa usalama kumfungulia mashtaka kwa madai ya kuwa kitendo chake cha kampeni kingeliweza kusambaza virusi vya corona.

Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi alikamatwa Jumatano alipokuwa anafanya kampeni zake upande wa mashariki mwa Uganda na hatua hiyo ilizusha maandamano makubwa yaliyo sababisha vifo vya watu 37 kulingana na taarifa za polisi.

Maafisa wa usalama wanasema wanajeshi walipelekwa katika sehemu mbali mbali za mji mkuu wa Kampala na maeneo ya karibu kuwasaidia polisi kuwatawanya waandamanaji.

Inaripotiwa kwamba wanajeshi na polisi wametumia risasi na mabomu ya kutoa machozi katika juhudi za kuzima maandamano.

Msemaji wa polisi Fred Enanga anasema watu waliokamatwa walihusika katika ghasia pamoja na kuwashambulia watu wasio wafuasi wa chama cha Bobi Wine cha NUP.