Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 21:41

Watu 16 wamekufa, 65 kujeruhiwa, zaidi ya 350 wamekamatwa Uganda


Polisi watumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji Kampala, Uganda
Polisi watumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji Kampala, Uganda

Polisi nchini Uganda wamesema kwamba watu 16 wamefariki na 65 kujeruhiwa kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu Bobi wine.

Msemaji wa polisi jijini Kampala Patrick Onyango amesema kwamba zaidi ya watu 350 wamekamatwa.

Viongozi wa chama cha Bobi Wine wamesema kwamba polisi wamekataa mtu yeyote kuonana naye anapozuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya mjini Jinja, mashariki mwa Uganda.

Nalufenya ni kituo cha polisi chenye historia ya ukandamizaji mkubwa wa haki za kibinadamu, ambapo washukiwa wa makosa makubwa kama ugaidi huzuiliwa.

Barabara kuingia katikatija mji mkuu Kampala zimefungwa huku idadi kubwa ya polisi na wanajeshi wakishika doria.

Waziri wa habari ametoa taarifa inayomsifu Rais Yoweri Museveni, namna anavyokabiliana na waandamanaji na kutoa wito kwa raia kuwatambua watu wanaofanya vurugu, kuwakamata na kuwapeleka polisi.

Msemaji wa polisi Patrick Onyango, amesema kwamba waliokamatwa walikuwa wanaharibu mali, wizi, kuchochea ghasia, kuwapiga polisi mawe na kushiriki maandamano kinyume cha sheria.

Wagombea kadhaa wa urais kupitia vyama vya upinzani wamesitisha kampeni zao hadi Bobi Wine atakapoachiliwa huru.

Wagombea 10 wa urais wanatarajiwa kukutana leo Ijumaa kujadiliana kuhusu hatua ya kuchukua.

Uchaguzi wa Uganda umepangwa kufanyika Januari 14 mwaka ujao 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG