Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Januari 14, 2025 Local time: 05:26

Wagombea wa urais Uganda wasitisha kampeni hadi Bobi Wine aachiliwe huru


Mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, ambaye pia anajulikana kama Bobi Wine akiwa katika gari la polisi baada ya kukamatwa wilayani Luuka mashariki mwa Uganda, Nov. 18, 2020.
Mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, ambaye pia anajulikana kama Bobi Wine akiwa katika gari la polisi baada ya kukamatwa wilayani Luuka mashariki mwa Uganda, Nov. 18, 2020.

Wagombea wakuu wa urais kupitia vyama vya upinzani nchini Uganda wametangaza kusitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine atakapoachiliwa na polisi.

Wagombea hao wakiwemo waliokuwa majenerali katika jeshi, wamesema kwamba hawawezi kuendelea kufanya kampeni wakati mgombea mwenzao anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi na kinyume cha sheria.

Wamesitisha kampeni kuanzia Jumatano, baada ya Bobi Wine kukamatwa akiwa katika kampeni mashariki mwa Uganda katika wilaya ya Luuka.

Taarifa ya polisi inasema kwamba Bobi Wine amekamatwa kwa kushindwa kuzingatia maagizo ya tume ya uchaguzi namna ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona kwa kuandaa mkutano wa kampeni wenye zaidi ya watu 100.

Maandamano yalitokea jumatano katika sehemu kadhaa za Uganda baada ya Bobi Wine kukamatwa.

Polisi wanasema watu 3 wameuawa na 34 kujeruhiwa katika maandamano hayo.

Polisi walitumia risasi za moto na gesi ya kutoa machozi kukabiliana na waandamanaji waliokuwa na hasira.

Bobi Wine anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya, wilayani Jinja.

Patrick Amuriat – FDC

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha Forum for democratic change Patrick Amuriat naye alikamatwa mjini Gulu, kuzuiliwa kwa muda kabla ya kuachiliwa huru.

Kulingana na polisi, Amuriat alikuwa amekiuka maagizo ya tume ya uchaguzi ya namna ya kufanya kampeni katika mazingira ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona.

Amuriat alikuta uwanja ambapo alikuwa amepangiwa kufanya kampeni ukiwa umezingirwa na polisi na kumzuia pamoja na wafuasi wake kuingia uwanjani.

Ni mara ya tatu polisi wamemkamata Amuriat akiwa katika kampeni kaskazini mwa Uganda.

Jenerali Mugisha Muntu – ANT

Mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Alliance for national transformation ANT, Generali Mugisha Muntu, amekemea hatua ya kukamatwa kwa Bobi Wine na kutaka aachiliwe haraka.

Ametangaza kusitisha kampeni hadi Bobi Wine atakapoachiliwa huru na kutoa wito kwa raia wote wa Uganda kuishinikiza serikali kumwachilia huru.

“Maafisa wa usalama wanaendelea kukaidi sheria na kuendelea kuwahangaisha wanasiasa wa upinzani. Hatua yao inaisukuma nchi hiii hadi hatua ya kuvunjika. Kama mgombea wa urais anaweza kukamatwa kwa njia hii, raia wa Uganda wanastahili kujiuliza kile kinachoweza kuwafanyika.” Amesema Muntu.

Jenerali Henry Tumukunde – mgombea huru

Mgombea huru na ambaye alikuwa waziri wa usalama kabla ya kufutwa kazi mwaka 2018 Jenerali Henry Tumukunde amesema kwamba Uganda imefikia kiwango cha kubadilisha historia.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Tumukunde amesema kwamba mazingira ya kisiasa nchini Uganda yameendelea kuwa magumu na hata wagombea wa urais hawawezi kufanya kampeni na kuwasilisha ujumbe wao kwa wapiga kura.

Ameendelea kusema kwamba anafanya mazungumzo na viongozi wenzake, ili wakubaliane la kufanya.

“Nimefikia uamuzi wa kusitisha kampeni mara moja hadi mgombea mwenzangu atakapoachiliwa na maafisa wa usalama kuacha kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia ambao wanataka mabadiliko kwa njia ya amani.” Ameandika Jenerali Tumukunde.

Nobert Mao – DP

Mgombea wa urais kupitia chama kikongwe cha Democratic party – DP, Nobert Mao ametoa taarifa kwa vyombo vya habari akiwataka wanasiasa wote na watetezi wa demokrasia kuingilia kati na kuhakikisha kwamba Bobi Wine anaachiliwa huru.

“Nimewaomba wanasheria wetu kuchukua hatua za haraka kulingana na sheria na kuhakikisha kwamba Robert Kyagulanyi anaachiliwa haraka iwezekanavyo.” Amesema Mao.

Dr. Kiiza Besigye

Aliyekuwa mgombea mara nne wa urais dhidi ya rais Yoweri Museveni Dr. Kiiza Besigye, ameandika kwenye twiter kwamba “inasikitisha kwamba tume ya uchaguzi imekaa kimya wakati wagombea wa urais wanakandamizwa na maafisa wa usalama. Hili litasababisha hali mbaya na majuto.”

Besigye anataka wagombea wote wa urais kukutana na kujadiliana namna ya kuendelea na kampeni.

Besigye alijiondoa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Januri 14, mwaka ujao 2021.

Alisema kwamba ni vigumu kumshinda rais Yoweri Museveni kwa sababu ataiba kura.

Kampeni ya Rais Museveni

Wakati wanasiasa wa upinzani wanakamatwa kwa kukiuka maagizo ya tume ya uchaguzi namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona, mwanamuziki Moses Ssali, maarufu Bebe Cool, anaendelea kuvutia umati wa watu akimfanyia kampeni rais Yoweri Museveni, bila mikutano yake kuvunjwa na maafisa wa usalama.

Rais Museveni anaendelea kukutana na wagombea wa viti mbalimbali katika kampeni yake ambayo ameitaja ya kisayansi nila kuwepo umati mkubwa wa watu.

Mikiutano yake yote inapeperushwa kwenye stesheni za radio katika sehemu anazoenda, Pamoja na runinga ya taifa, UBC.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG