Polisi nchini Uganda wamesema Jumanne kuwa wanachunguza endapo kundi la kigaidi la al-Shabab lilihusika katika mauaji ya mwendesha mashitaka mjini Kampala Jumatatu.
Joan Kagezi, mwendesha mashitaka katika kesi inayoendelea kuhusu watu zaidi ya 12 wanaokabiliwa na mashitaka ya ugaidi, huenda alilengwa kutokana na kazi yake, alisema msemaji wa polisi Patrick Onyango.
Ubalozi wa Marekani mjini Kampala umelaani mauaji ya mwendesha mashitaka huyo katika taarifa yake Jumanne na kumwelezea Kagezi kama "shujaa aliye msitari wa mbele katika kupambana na uhalifu na ugaidi."
Polisi inasema Kagezi alipigwa risasi mara mbili na watu wenye bunduki Jumatatu jioni wakati anatoka katika gari lake akiwa na watoto wake wawili nje kidogo ya Kampala. Baada ya kumpiga risasi kichwani na shingoni washambuliaji hao walitoroka kwa kutumia piki piki.
Mauaji hayo yameshtua Uganda huku kukiwa na ilani za mara kwa mara kuhusu mashambulizi ya kigaidi nchini humo.