Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini yaandikisha wafungwa kupiga kura

Mafisa wa tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini wakisubiri watu wajiandikishe kupiga kura mjini Johannesburg. November 18, 2023.

Maafisa wa uchaguzi wa Afrika Kusini wametembelea jela kote nchini , kama sehemu ya kuandikisha takriban wafungwa laki moja, ili washiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

Katiba ya Afrika Kusini inatoa haki kwa kila mmoja aliyefikisha umri, kushiriki kwenye upigaji kura, ikiwa na maana kwamba wafungwa pia wana haki ya kushiriki zoezi hilo, kinyume na ilivyo kwa mataifa mengine ya kiafrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, tarehe kamili ya uchaguzi huo haijatangazwa, ingawa unatarajiwa kufanyika kati ya Mei na Agosti mwaka 2024. Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini inalenga kuandikisha idadi kubwa zaidi ya wafungwa kwenye jela 240 zilizopo kote nchini, ili wapige kura kwenye uchaguzi huo.

Takriban wafungwa 15,000 walishiriki kwenye uchaguzi uliomalizika 2019. Sasa hivi taifa hilo lina takriban wafungwa 157,000 waliopo jela, kulingana na mamlaka, wakati likikabiliana na mojawapo ya viwango vya juu vya uhalifu ulimwenguni.