Wakati huo huo viongozi wa majimbo hayo wanamtaka rais kushughulikia kwa dhati tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa, ambalo wanasema ni chanzo cha moto huo mkubwa kuwahi kushuhudiwa hapa nchini.
Rais Trump atakutana na viongozi wa California Jumatatu ili kufahamishwa juu ya hasara zinazotokana na moto wa msitu uliokwisha sababisha vifo vya zaidi watu 30, wengine kadhaa hawajulikani walipo na maelfu wamelazimika kuhama makazi yao.
Zaidi ya miji 6 imeteketea kabisa pamoja na karibu hekta milioni moja ya misitu kuungua katika majimbo ya California Washington na Oregon.
Mpinzani wa rais Trump kwenye uchaguzi wa Novemba 3 Joe Biden atazungumzia suala la mabadiliko ya hali ya hewa kutoka nyumbani kwake Delaware Jumatatu, akijaribu kuweka mbele suala la mabadiliko ya hali ya hewa.
Gavana wa Jimbo la California Gavin Newsom akizungumzia janga hilo wiki ilyiopita alisema : "Hii bila shaka ni dharura ya mabadiliko ya hali ya hewa. Jambo hilo kwa hakika linatendeka. Linatendeka kwa hali ambayo haijawahi kushuhudiwa mwaka bada ya mwaka."
Rais Trump aliiondowa Marekani kutoka mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya hali ya hewa akidai ni ghali kutekeleza na kutoamini kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanatokea.
Akihutubia mkutano wake wa kwanza ndani ya ukumbi hapo jana mjini Nevada licha ya kwamba maafisa wa jimbo hilo kukemea anakiuka kanuni za jimbo za kutofanyika mikusanyiklo mikubwa ya watu kutokananna janga la Corona, Trump alisisitiza tena kwamba moto unaoendelea ni kutokana na usimamizi mbaya wa misitu akiwakosoa magavana wa majimbo hayo kwa usimamizi huo mbaya.
Rais Trump : "Tunachokitaka ni usimamizi wa kweli wa misitu, tunahitaji usimamizi wa misitu. Utawala wangu unashirikiana kwa karibu na viongozi wa majimbo na gavana na unatoa shukurani kwa wazima moto 28,000 wanaokabiliana kwa ushujaa na moto huo."
Wabunge wa majimbo ya Washington na Oregon hawakubaliani kamwe na hoja hiyo ya rais.
Jeff Merkley ni seneta wa jimbo la Oregon anátema : "Unajua, rais amesema hii inatokana na uharibifu wa misitu. Huo ni uwongo mtupu. Tuna theluji inayopunguka milimani. Misitu yetu inazidi kukauka. Bahari imezidi kuwa na joto. Na mambo haya yamekuwa yakitokea pole pole kwa miongo kadhaa sasa. Itakuaje si mabadiliko ya hali ya hewa?"
Viongozi wa majimbo hayo ya magharibi wanataka hatua za dharura zichukuliwa kukabiliana na mabadliko ya hali ya hewa. Huku baadhi ya watetezi wa mazingira wakilalamika kwamba mgombea kiti cha urais wa chama cha Demokrati Joe Biden hajaliweka suala hilo juu katika ajenga yake.
Ndio maana wachambuzi wanasema Biden atalizungumzia suala hilo hii leo baada ya kutoa tarifa Jumapili inayotoa wito kwa watu kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.