Trump alitoa matamshi hayo saa chache baada ya kukutana na Zelenskiy mjini Paris katika mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana tangu Trump kushinda uchaguzi wa mwezi uliopita.
Trump aliapa kusukuma mazungumzo ya kumaliza mzozo huo, lakini hajaweza kutoa maelezo zaidi kufikia sasa.
“Zelenskiy na Ukraine wanataka kufikia makubaliano ili kumaliza vita hivi visivyo na maana,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akiongeza kuwa Kyiv imepoteza takriban wanajeshi 400,000.
“Lazima kuwe na sitisho la mapigano la mara moja na mazungumzo yanapaswa kuanza,” Trump alisema.
Trump alikutana kwa mazungumzo ya saa moja na Zelenskiy Jumamosi mjini Paris, wakati wa hafla ya kufungua tena kanisa ya Notre Dame.
Akijibu kuhusu ujumbe wa Trump Jumapili, Zelenskiy alisema amani sio tu maneno, kunahitajika dhamana.
“Tunapozungumzia amani ya kudumu na Russia, lazima tuzungumzie kwanza dhamana ya kudumu kwa ajili ya amani. Wananchi wa Ukraine wanataka amani kuliko mtu yeyote yule,” aliandika kwenye mtandao wa X.