Mchapishaji wa tovuti ya Newsmax , Christopher Ruddy- ambae ni rafiki wa Trump- ameandika Jumapili kwamba rais amemwambia “ Hili suala litachunguzwa. Yote hayo yatakuja kujitokeza. Itakuja kujulikana niko sahihi.
Ruddy amesema hajawahi kumuona Trump amekasirika kwa muda mrefu.
Rais wa Marekani Donald Trump pia ameshinikiza kuwa jopo linalosimamia usalama katika Bunge la Congress lichunguze iwapo uongozi wa Rais Barack Obama ulitumia vibaya mamlaka yake.
Amelitaka Bunge kufanya uchunguzi juu ya yale yaliojiri kabla ya uchaguzi wa rais Novemba iliyopita, ikiwa ni sehemu ya madai kwamba Russia ili ingilia kati upigaji kura.
Bila ya ushahidi wowote, Trump amemshutumu Obama Jumamosi kuwa alihusika katika udukuzi wa mawasiliano yake huko kwenye makao makuu ya Jengo lake la Trump Towers, New York mwezi mmoja kabla ya uchaguzi, madai ambayo msaidizi wa rais mstaafu amekanusha kuwa ni “uwongo tu.”
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa James Clapper amekiambiakituo cha televisheni cha NBC; katika kipindi chake Meet the Press Jumapili, “Hakuna udukuzi wowote uliofanyika dhidi mazungumzo ya simu ya rais mteule wakati huo, au alipokuwa mgombea wa urais au hata kwa kampeni yake.”
Clapper amesema hakuna amri ya mahakama yoyote iliokuwa imeruhusu udukuzi dhidi ya Trump kabla au baada ya uchaguzi.
“Ripoti zakuwepo uwezekano wa njama za kisiasa kufanya udukuzi wakati huo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2o16 zinatia wasiwasi,” msemaji wa White House Sean Spicer.
Wajumbe wa Congress, wa pande zote Demokrat na Republikan, wamekosoa madai ya Trump kwamba kulifanyika udukuzi au wamedadisi iwapo ana ushahidi wowote.