Siku mbili baada ya wafuasi wa Trump wenye hasira kuvamia Bunge la Marekani wakati kikao cha kurasimisha ushindi wa Biden, Trump ameandika, “Mimi sitahudhuria sherehe za kuapishwa Januari 20.”
Chini ya siku moja, Rais Trump alitoa picha ya video akiahidi kutumia muda wake uliobaki akiwa madarakani “kufanikisha makabidhiano ya madaraka kwa utulivu, wepesi bila ya migogoro yoyote” kwa Biden.
Trump atakuwa ni rais wa kwanza wa Marekani tangu Andrew Johnson kutohudhuria sherehe za kuapishwa rais. Johnson hakuhudhuria kuapishwa kwa mrithi wake miaka 152 iliyopita.
Hata baada ya kukubali Alhamisi kuwa Biden ataingia ofisini mwezi huu kwa kuchelewa kufanya hivyo muda mrefu, Trump ameendelea kusisitiza kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi wa awamu yake ya pili.
Maafisa katika utawala wake – akiwemo Mwanasheria Mkuu wa zamani, William Barr – wamethibitisha kutokuwepo ushahidi wa kutosha wa wizi wa kura ambao ungemfanya Trump kushinda uchaguzi huo.