Trump asema amewapiku marais wengine wa Marekani

Rais Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump ameadhimisha siku ya 500 katika madaraka Jumatatu, akitangaza kuwa “wengi wanaamini” kwamba ameweza kutekeleza mambo mengi zaidi kuliko rais wengine wa Marekani.

Trump alieleza punguzo la kodi lililopitishwa mwaka jana, hatua iliyopigwa na jeshi la Marekani, kupungua kwa uhalifu na wahamiaji haramu, mipaka iliyodhibitiwa zaidi na kukua kwa uchumi ni kati ya mafanikio yake.

Hivi sasa katika mwezi wa 17 akiwa White House, Trump ameendelea kuwa mtu mwenye utata nchini Marekani wakati jumla ya kura za maoni za taifa zinaonyesha wapiga kura hawaridhiki na utendaji wake kwa asilimia 52.8 dhidi ya asilimia 44.4 inayoridhika naye.

Hivi sasa anakabiliwa na uchunguzi unaondelea mwaka mzima unaofanywa na mwendesha mashtaka maalum Robert Mueller kuhusiana na uhusiano uliokuwepo kati ya kampeni yake ya 2016 na Russia na iwapo alizuilia sheria kuchukua mkondo katika uchunguzi unaofanyika, na mara nyingi Trump amekanusha tuhuma za kushirikiana na Moscow na kuwa kipingamizi.

Katika ujumbe wake wa Twitter amesema, “Kama ilivyoelezwa na wanazuoni wa sheria mbalimbali, Ninayo haki kamili kujisamehe mimi mwenyewe, lakini kwa nini nifanye hivyo wakati sikufanya kosa lolote.?

Tajiri huyo mwenye biashara ya majumba ambaye amegeuka kuwa mwanasiasa wa Republikan anaendelea kuwa maarufu kati ya wapiga kura wa chama cha Republikan ambao walifanya ashinde na kuwa rais wa 45 wa nchi hii. Wapiga kura binafsi, na hasa Wademokrat, wanaendelea kupinga urais wake, kura za maoni zinaonyesha hivyo.