Trump aonya 'matokeo mabaya sana' iwapo Iran itaendelea na nyuklia

Chansela Angela Merkel

Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran Jumatano kuwa kutakuwa na “matokeo mabaya sana” iwapo itaanza kutengeneza silaha za nyuklia kufuatia Marekani kujitoa katika mkataba wa kimataifa wa 2015 uliokuwa unania ya kuizuia Tehran kuendeleza programu yake ya nyuklia.

Katika maoni mafupi aliyo yatoa White House, Trump amesema Marekani “muda mfupi ujao” itarejesha vikwazo vya uchumi katika juhudi za kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo mapya juu ya mkataba huo, ikiwa ni pamoja na majaribio yake ya makombora ya ballistic na harakati zake za kijeshi huko Syria, Yemen na maeneo mengine huko Mashariki ya Kati.

Kiongozi huyo wa Marekani ameituhumu Iran kwa kutengeneza “vurugu na vifo” katika eneo hilo.

“Sisi tutaingia katika mkataba mzuri sana au hatutakuwa na mkataba wowote,” amesema. Trump amekiri kuwa Marekani “huenda isifanye vizuri sana katika kufikia makubaliano,” lakini amesema hilo ni sawa kwa upande wake.

Trump ameendelea kuupiga vita mkataba wa nyuklia wa Tehran uliokuwa umefikiwa na Marekani aliosaini mtangulizi wake, Barack Obama, akiuita “mbaya, mkataba mbaya ambao ulitakiwa usiwepo kabisa.”

Maoni ya Trump yamekuja wakati nchi tano nyingine zilizosaini mkataba huo—Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Russia na China—wote wakipaza sauti zao kuwa wanaunga mkono upya mkataba huo.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kujiondoa kwa Marekani kutoka katika mkataba huo wa 2015 ni jambo la kusikitisha na kuwa Berlin “itajaribu kufanya kila inaloweza ili Iran itekeleze ahadi yake siku za usoni.”

Amesema kuwa kitendo cha Trump kususia mkataba huo “inaonyesha kwa mara nyingine kuwa tutakuwa na majukumu zaidi katika bara la Ulaya, katika sera za kigeni, katika masuala ya kutafuta amani, na masuala yanayotulazimu kutafuta suluhu za kisiasa.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Boris Johnson ameishauri Marekani “kuacha kuchukua hatua yoyote ambayo itazuilia pande nyingine zilizoshiriki katika mkataba huu kuendelea kufanya makubaliano haya yawe na tija,” akisema kuwa mkataba huu ni “Muhimu” kwa ajili ya usalama wa taifa la Uingereza.

Johnson amesema ni juu ya uongozi wa Marekani kuonyesha jinsi wanavyotaka jambo hili liendelee.”

Ikulu ya Kremlin imesema Rais wa Russia Vladimir Putin ameeleza “wasiwasi wake mkubwa juu ya uamuzi wa Trump na mara nyingine amesisitiza umuhimu wa mkataba huu,” wakati Ufaransa na China pia imepaza sauti kuunga mkono mkataba huo uendelee na Iran.