Mkutano huu unakuja miezi kadhaa baada ya Trump kumtuhumu Merkel kuwa "ameiangamiza" Ujerumani kwa kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi wa Syria kuingia nchini.
Angela Merkel na Donald Trump walikuwa wamepangiwa kukutana mapema wiki hii, lakini hali ya theluji upande huu wa Pwani ya Mashariki ya Marekani ilisababisha viongozi hao wawili kuuchelewesha mkutano wao.
Huu utakuwa ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kati ya viongozi hao wawili wa kitaifa tangia Trump aibuke kidedea bila ya kutarajiwa katika uchaguzi wa urais wa Novemba mwaka jana.
Kabla ya uchaguzi huo, Trump alisema kuwa uamuzi wa Merkel wa kuwakubali wakimbizi ulikuwa ni “kosa lililoleta janga kubwa” na alimtuhumu kuwa alikuwa “aniangamiza Ujerumani.”
Trump amezitaka nchi za NATO kulipa michango yao kwa ajili ya mahitaji ya ulinzi wao.
Merkel, mwenye uwezo wa ushawishi mkubwa Ulaya, amekuwa akikosoa makatazo ya kusafiri alioyitoa dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, ambayo yamezuiliwa na mahakama za Marekani.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa hata hivyo Trump pengine akataka ushauri kutoka kwa Merkel wakati wakiwa kwenye ofisi ya Oval wanapokutana, juu ya njia bora ya kushirikiana na Rais wa Russia Vladimir Putin.
Merkel amekuwa akikabiliana na kiongozi huyo wa Russia mwenye utata, wakati Trump amekuwa akimsifia, kitu kilichopelekea wabunge wa Republikan na Demokrat wa Marekani kuwa na wasiwasi mkubwa.