Baada ya zaidi ya miaka tisa madarakani, uungwaji mkono wa Trudeau ndani ya chama chake tawala cha Liberal ulianza kushuka mwaka 2024 kutokana na kuongezeka kwa ukosoaji wa umma kwa sababu ya kupanda kwa gharama ya maisha.
Mamlaka yake ilitikiswa na kuondoka ghafla kwa waziri wa fedha na naibu waziri mkuu Chrystia Freeland mwezi uliopita.
“Nina nia ya kujiuzulu kama kiongozi wa chama, kama waziri mkuu, baada ya chama kumchagua kiongozi ajaye,” Trudeau aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Ottawa kufuatia mzozo wa kisiasa unaoendelea polepole ambao ulisababisha washirika wake wakuu katika chama cha Liberal kumtaka ajiuzulu.
Haikufahamika mara moja, ni kwa muda gani Trudeau ataendelea kubaki madarakani kama waziri mkuu wa mpito.
Alisema mchakato wa kumchagua kiongozi wa chama cha Liberal “utakuwa thabiti na wenye ushindani kitaifa.”
Hiyo inamaanisha Trudeau ataendelea kuiongoza Canada hadi rais mtarajiwa wa Marekani Donald Trump atakapoingia rasmi madarakani mwezi huu na atakuwa na jukumu la kusimamia majibu ya awali ya nchi yake kwa utawala mpya wa Marekani, ikiwemo kukabiliana na uwezekano wa vita vya kibiashara.
Trump aliapa kuweka ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa zote zinazoagizwa kutoka Canada, hatua ambayo inaweza kuathiri vibaya uchumi wa nchi hiyo, na Trudeau alikuwa ameahidi kulipiza kisasi.