TCRA-Tanzania yaanza kushughulikia 'kero' ya rais

Nembo ya TCRA

Zoezi la kuanza kuvisajili vyombo vya habari nchini ikiwemo mitandao ya jamii linaanza Jumatatu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza Jumamosi, ikiwa ni hatua ya kushughulikia 'kero' zinazohusishwa na mitandao ya jamii.

Mamlaka hiyo imesema wahusika wanapaswa kujisajili kabla ya Mei 5, mwaka 2018, kwa mujibu wa kanuni ya nne ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2018.

Mwezi Aprili wakati Rais John Magufuli akiwaapisha Majaji wapya 10, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka , alisema kuna ugonjwa ambao umeingia nchini wa watu kudhani kwamba kila kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni cha kweli.

Alisema hayo yote yamesababishwa na uhuru wa watu kutuma vitu kwenye mitandao hiyo bila kudhibitiwa.

Rais Magufuli alisema kwa kuwa Tanzania haina uwezo wa kuidhibiti mitandao hiyo, wako watu nje ya nchi ambao wanaitumia kwa maslahi yao bila kujali madhara yanayoweza kutokea.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kila mwombaji atatakiwa kulipa ada ya maombi shilingi 100,000 ambayo haitarudishwa.

Taarifa hiyo ilivitaja vyombo hivyo kuwa ni vya blogs, majukwaa ya mitandaoni, redio na televisheni zinazotangaza kupitia mitandaoni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ambayo imenukuliwa na gazeti la Nipashe nchini Tanzania waombaji watakaokidhi vigezo na masharti ya usajili, watajulishwa ili walipie ada ya mwanzo ya leseni na kupewa leseni zao.

“TCRA imepewa dhamana ya kuandaa na kutunza Rajisi ya watoa huduma za maudhui kupitia blogu, majukwaa mtandaoni, redio na televisheni mtandaoni, kuchukua hatua kunapotokea ukiukaji wa kanuni tajwa na pia kuelimisha umma kuhusu kanuni hizo,” taarifa hiyo imeeleza.