Mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa Serikali kutoka Tanzania na China na wawakilishi wa vyombo vya habari Jumanne.
Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa Mkutano huo ulikuwa ukijadili matumizi mabaya ya mtandao yanayoweza kuleta madhara katika vyombo vya habari.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani amesema sheria ya udukuzi wa kimtandao inayotumika nchini haina uwezo wa kuwawajibisha watu wanaotumia vibaya mtandao kutokana na tofauti za tamaduni.
“Sasa tuna watu wanaodhibiti wahalifu wa kimtandao, lakini wanapata wakati mgumu kuthibitisha ushahidi kupitia mitandao ya kijamii kwa sababu mingi inatoka Marekani na kusimamiwa na sheria za nchi hiyo,” amesema Ngonyani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa katika mkutano huo Tanzania ni moja kati ya nchi barani Afrika ambayo matumizi ya kimtandao yanakua kwa kasi.
Balozi wa China nchini TanzaniaLu Youqing amesema kwa sababu hiyo ni lazima kuwe na udhibiti wa watumiaji wabaya wamitandao.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuna ongezeko la mara 13.7 kwa watumiaji wa simu ndani ya miaka 10 kutoka milioni 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia watu milioni 39.8 mwaka 2015.
Aidha watumiaji wa tovuti walifikia milioni 17.26 mwaka 2015 kutoka milioni 1.01 mwaka 2005.