Takriban watu 100 wauwawa Kabul, 163 wajeruhiwa

Polisi nchini Afghanistan wakikagua eneo la tukio la shambulizi la bomu mjini Kabul.

Takriban watu 100 wameuwawa katika shambulio la bomu la kujitoa muhanga lililotokea mjini Kabul Jumamosi na wengine zaidi ya 163 wajeruhiwa. Serikali ya Afghanistan imesema kuwa Jumapili ni siku ya maombolezo, wakati mazishi ya wahanga wa tukio hilo na msako wa manusura ukiendelea.

Mshambuliaji alitumia gari la ambulance lililokuwa limejaa vilipuzi na kupita kwenye kizuizi cha polisi hadi kuwafikia watu waliokuwa wamekusanyika katika eneo lenye makazi yenye majengo mengi ya serikali na balozi.

Kundi la Taliban mara moja lilidai kuhusika na kupanga shambulizi hilo.

Msemaji wa kikundi hicho amesema kuwa shambulizi hilo lililenga kikundi cha maafisa wa kikosi cha ulinzi cha Afghanistan.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo ya usalama shambulizi hili ni kubwa zaidi likilinganishwa na lile ambalo lilitokea lililotokea kwenye hoteli moja mjini Kabul ambapo watu 22 waliuawa wiki moja iliyopita.

Nayo Ikulu ya White House imetoa tamko Jumamosi kulaani shambulizi hilo.

“Kitendo hiki cha kinyama kinarudisha azma yetu mpya kwa upande wa Marekani na Washirika wetu wa Afghanistan. Ukatili wa Taliban hautaruhusiwa kuendelea. Marekani imejizatiti kuifanya Afghanistan ambayo ni huru kutokana na makucha ya magaidi ambao wanadhamiria kuwashambulia Wamarekani, washirika wetu na mtu yoyote ambaye hakubaliani na itikadi zao,” tamko hilo limesema.

Kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa tamko, linalosema: “Kitendo cha Taliban kutumia gari ya ambulance kama silaha kuwashambulia raia inaonyesha namna wasivyo wathamini wananchi wa Afghanistan na wote wale wanaoshiriki kuleta amani nchini humo, na uvunjifu wa desturi za msingi wa juu wa kimataifa. Tunawapongeza wafanyakazi wa huduma za dharura kwa ushujaa wao katika kukabiliana na shambulizi hili la kigaidi.”

Matamko yote mawili yamezitaka nchi zote zinazo isadia Afghanistan “kufanya maamuzi ” ya kuzuia misaada kwa makundi ya kigaidi na Taliban.