Syria haitoingilia kati tena katika masuala ya Lebanon, asema kiongozi mpya

Kiongozi wa jamii ya Lebanon ya Druze akikutana na kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa, mjini Damascus, Disemba 22, 2024. Picha ya Reuters

Kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa Jumapili amewambia viongozi wa jamii ya walio wachache nchini Lebanon ya Druze kwamba nchi yake haitoingilia kati kwa nia mbaya katika masuala ya Lebanon na kwamba itaheshimu uhuru wa jirani yake.

Syria haitoingilia kati kamwe kwa nia mbaya katika masuala ya Lebanon, inaheshimu uhuru wa Lebanon, umoja wa maeneo yake, uhuru wa maamuzi yake pamoja na usalama na utulivu wake,” Sharaa amewaambia viongozi wa jamii ya Druze Walid na Taymur Jumblatt.

Walid Jumblatt ni kiongozi wa kwanza wa Lebanon kukutana na Sharaa tangu kundi lake la Kiislamu Hayat Tahrir al-Sham na makundi ya waasi washirika wake kuanzisha mashambulizi mwezi uliopita, na kuuteka mji wa Damascus tarehe 8 Disemba na kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Bashar al-Assad.

Walid Jumblatt, mkosoaji mkubwa wa muda mrefu wa Assad na baba yake Hafez ambaye aliiongoza Syria kabla ya mwanawe, aliwasili Damascus Jumapili akiongoza ujumbe wa wabunge na viongozi wa kidini kutoka jami ya walio wachache nchini Lebanon ya Druze.