Shirika hilo limesema kuwa limeorodhesha visa 12 ambapo serikali ya Misri ilirejesha jumla ya raia 800 wa Sudan kati ya Januari na Machi mwaka huu, bila kuwapa nafasi ya kuomba hifadhi, au kujitetea dhidi ya kurejeshwa.
Ripoti zimeongeza kusema kuwa pia limeorodhesha kesi 27 za wakimbizi wa Sudan waliokamatwa kati ya Okotoba 2023 na Machi 2024, ishirini na sita wakiwa miongoni mwa wale waliofukuzwa nchini, baada ya kuzuiliwa kwenye mazingira magumu kabla ya kuondolewa nchini.
Idadi kamili ya watu waliokamatwa au kurejeshwa makwao haijulikani kwa kuwa hakuna takwimu zilizotolewa kwa umma, ingawa Human Rights Watch limesema kuwa maelfu walirejeshwa makwao mwishoni mwa mwaka jana, wengi wao wakiwa ni kutoka Sudan.
Wizara ya habari ya Misri bado haijatoa majibu kutokana na madai hayo. Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, zaidi ya watu 500,000 ambao ni takriban asilimia 24 ya watu waliotoroka Sudan baada ya mapigano kuzuka, waliingia Misri.