Idadi ya wale waliouawa kutokana na mlipuko huo imeongezeka kufikia watu 14, na dazeni za watu kadhaa wengine wamejeruhiwa na wako katika hali mbaya.
Polisi wa Russia wametoa picha ya mshukiwa aliyejilipua Dzhalilov, 22, ambaye wamesema alizaliwa huko Osh na kuwa raia wa Russia mwaka 2011.
“Ndio, kamati ya serikali ya usalama wa taifa imethibisha hilo, kwa kutumia takwimu za mwanzoni, kwamba aliyejilipua alikuwa anaasili ya Kyrgyz, ambaye alichukuwa uraia wa Russia,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Kyrgyzstan, Erlan Abdyldaev wakati akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov huko Moscow.
Wapelelezi wa Russia wanasema Dzhalilov aliweka bomu la pili katika kituo kingine cha treni katika mji wa St Petersburg ambalo polisi waliligundua na kuzuia lisiripuke. Hakuna kikundi mpaka sasa kilichodai kuhusika na shambulizi hilo lakini vyombo vya serikali vinachunguza uwezekano wa kuwepo mahusiano na kikundi cha Islamic State.
Viongozi wa ulimwengu kutoka China mpaka Ulaya hadi Brazil wametuma rambirambi zao juu ya tukio hilo la mauaji. Rais Donald Trump ameongea kwa simu na Rais wa Russia Vladimir Putin na kumhakikishia kumsaidia ipasavyo katika kukabiliana na shambulizi hilo.