Marekani yawaenzi Mashujaa wake siku ya 'Memorial Day'

Makaburi yawekewa bendera ya taifa kama ni sehemu ya kuwaenzi mashujaa huko Arlington.

Siku ya Mashujaa (Memorial Day) nchini Marekani inasherekewa kote nchini leo Jumatatu.

Siku ya Mashujaa inaadhimishwa siku ya Jumatatu ya mwisho ya Mwezi Mei, na imetengwa kitaifa kuwaenzi wale wote waliokufa katika kuhudumia shughuli za kijeshi katika historia yote ya Marekani.

Bunge la Marekani lilitangaza siku ya mashujaa kuwa ni mapumziko rasmi kitaifa mnamo mwaka 1971.

Maadhimisho mbali mbali nchini na katika Jiji la Washington yanapangwa kwa ajili ya siku hii.

Ingawaje sio rasmi, siku hii inajulikana pia kuwa ni mwanzo wa kipindi cha joto kwa Wamarekani wengi.

Katika Jiji la Washington, Rais Donald Trump atajumuika katika sherehe za kuweka shada la maua katika makaburi ya Tomb of the Unknown Soldier huko katika makaburi ya Arlington ya kitaifa.

Kikundi cha Rolling Thunder wanashiriki katika sherehe za kuweka maua katika maeneo ya World War Two Memorial na Vietnam Memorial. Kikundi hiki huendesha pikipiki katika maeneno mbalimbali ilikuamsha hisia juu ya wale wanaoendelea kushikiliwa kama wafungwa wa kivita na wale ambao haijulikani wamepotelea wapi wakati wakiwa katika medani za vita.

Taasisi ya Veterans for Peace itakuwa na shughuli mbalimbali Washington kupinga kile wanachosema ni “pendekezo la bajeti linalokera sana la Rais Trump, ikiwemo kero ya ongezeko la dola za Marekani bilioni 54 kwa ajili ya wizara ya ulinzi.”

Siku ya Mashujaa ilianza mwaka 1865, baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani, wakati kikundi cha watumwa walioachiwa huru walipoadhimisha kile kinachojulikana kama ni kumbukumbu ya kwanza ya kitaifa ya wale waliokufa katika vita.

Kikundi hicho kilifukuwa miili zaidi ya 250 ya wanajeshi wa muungano kutoka katika kaburi waliozikwa pamoja katika jela ya kitaifa huko Charleston, South Carolina na kuwapa heshima ya maziko yanayostahili.

Kwa zaidi ya miaka 50, sikukuu hii ilikuwa tu inawakumbuka wale waliouawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na sio katika migorogoro mingine iliyohusisha Marekani kupeleka wanajeshi wake.

Lakini ni pale tu Marekani ilipoingia katika Vita ya Kwanza ya Dunia huu utamaduni ulianza kuwaenzi wale waliokufa katika vita za aina zote.

Mwaka huu, Siku ya Mashujaa inaadhimishwa sambamba na miaka mia moja ya kuzaliwa kwa rais wa 35 wa Marekani- John Fitzgerald Kennedy.

Kituo cha Kennedy kilichoko Washington kwa ajili ya Sanaa za maigizo kinafanya maadhimisho maalum ya miaka mia ya uzao wa JFK. Waigizaji Martin Sheen, Brian Dennehy na Soprano Renee Fleming ni kati wa wasanii watakao shiriki katika sherehe hizo.