Shambulio la anga la Israel laua watu wanne kusini mwa Lebanon

Watu wakitizama eneo la shambulizi la anga la Israel lililolenga nyumba moja katika kijiji cha Jibshit kusini mwa Lebanon, Februari 27, 2024. Picha ya AFP

Shambulio la anga la Israel Jumapili liliua watu wanne wa familia moja katika nyumba kwenye kijiji cha mpakani kusini mwa Lebanon, vyanzo vya ulinzi na usalama wa raia vimesema.

Watu hao wanne waliuawa katika kijiji cha Meiss al Jabal, ambacho kimekumbwa na uharibifu mkubwa katika majibizano ya mashambulizi ya mara kwa mara kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran tangu kuanza kwa vita huko Gaza Oktoba mwaka jana.

Katika taarifa, Hezbollah imesema ilirusha “darzeni” ya roketi aina ya Katyusha kwenye mji wa Israel wa Kiryat Shmona, mji wa kaskazini mwa nchi ulio karibu na mpaka wa Lebanon, katika shambulio la kulipiza kisasi.

Zaidi ya wanachama 250 wa Hezbollah na raia 75 wameuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon tangu Oktoba, vyanzo vya usalama huko vinasema.

Nchini Israel, shambulio la kombora kutoka Lebanon limeua takriban wanajeshi kumi na raia kadhaa, vyanzo vya Israel vinasema.