Mapema mwezi huu (Mei), asasi sita za kiraia ziliwasiilisha hoja mahakamani inayotaka kanuni hizo zisitishwe kwa muda. Wanaharakati wameushutumu uamuzi huo wa mahakama kuwa ni shambulizi dhidi ya uhuru wa kujieleza.
Kanuni hizo mpya zinawataka wamiliki wa mitandao kulipa ada ya hadi dola $900 za Kimarakani, kutoa habari za wajasiriamali, uraia wa wamiliki, tajiriba ya wafanyakazi kati ya mengine.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watakaokiuka kanuni hizo huenda wakafungwa jela kwa miezi 12, kupigwa faini ya shilingi milioni tano au adhabu zote mbili.
Tayari wamiliki wa mitandao na tovuti mbalimbali wameanza kusitisha huduma zao kwa kuhofia kukamatwa.
Baadhi ya wanaharakati wanamshutumu rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli, na kusema kuwa utawala wake umechukua hatua hiyo kwa sababu unaogopa kukosolewa.
Magufuli aliingia mamlakani mwaka wa 2015 kwa ahadi kwamba angeharakisha juhudi za kuimarisha uchumi na kukabilina na ufisadi nchini humo.