Serikali ya Somalia imezuiya ndege mbili za kigeni zilizotua mjini Mogadishu jumanne zikiwa zimebeba pesa taslimu dola milioni 3.6
Waziri wa mambo ya ndani Abdi Shakur Hassan Farah ameiambia Sauti ya Amerika- VOA kwamba serikali iliwakamata wafanyakazi sita kutoka kwenye ndege hizo wakiwemo raia kutoka Marekani, Uingereza na Kenya.
Farah amesema serikali iliruhusu ndege kutua lakini mamlaka za usalama zilishtukia baada ya watuhumiwa kuhamisha visanduku kutoka ndege moja kwenda nyingine. Waziri huyo amesema maafisa wa usalama waligundua pesa taslimu kwenye visanduku hivyo.
Maafisa wamesema wanafanya uchunguzi kujua ni kwa nini ndege hizo zilibeba kiasi kikubwa cha pesa.
Ndege au helikopta hutumiwa kusafirisha malipo ya fidia kwa maharamia wa kisomalia ambao wanateka meli za kigeni nje ya pwani ya Somalia.
Kwa kawaida fedha za malipo ya fidia mara nyingi hudondoshwa kwa ndege kwenye kontena kwa maharamia walioko ardhini.