Serikali ya DRC yataka kurejesha adhabu ya kifo kwa wanajeshi wanaopatikana na hatia ya uhaini

Rais wa DRC Felix Tshisekedi akiapishwa kuongozo muhula wa pili kwenye uwanja wa michezo mjini Kinshasa, Januari 20, 2024.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina lengo la kurejesha adhabu ya kifo, ambayo ilisitishwa miaka 20 iliyopita, kwa wanajeshi wanaopatikana na hatia ya uhaini dhidi ya waasi wa M23, kulingana na ripoti ya baraza la mawaziri.

Hukumu za kifo hutolewa mara kwa mara na mahakama nchini DRC lakini zilibadilishwa kuwa za kifungo cha maisha gerezani tangu kuondolewa kwa hukumu ya kifo mwaka wa 2003.

Waziri wa sheria siku ya Ijumaa aliwasilisha barua kwa baraza la mawaziri kuhusu “kuondoa katazo la hukumu ya kifo kwa wanajeshi”, msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema.

Alisema “Katika lengo la kukomesha uhaini, Baraza la ulinzi lilimuomba Rais kuondoa katazo hilo kipindi hiki ambapo, nchi inakabiliwa na uchokozi kutoka Rwanda,” ambayo inakanusha madai ya kuwasaidia waasi wa M23.