Maafisa wa Rwanda daima wanadai hawahusiki kamwe na mzozo unaoendelea huko mashariki ya Congo. Naibu msemaji wa serikali ya Rwanda Alain Mukuralinda anasema, watasubiri na kuona ikiwa mapemndekezo hayo yataidhinishwa na serikali ya Kinshasa.
Tangazo hili limetolewa wakati kuna juhudi mpya za kumaliza mashambulizi yanayofanywa na waasi huko mashariki DRC zinaendelea baada ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Jumanne kutaka kupelekwa mara moja majeshi ya kikanda kujaribu kuzuia ukatili unaofanywa na waasi mashariki mwa DRC.
Rais wa Kenya ametoa wito huo baada ya shambulizi kubwa kufanywa na waasi wa M23 katika mashariki ya nchi hiyo Jumatatu iliyopita na kuchukua udhibiti wa mji wa Bunagana, wenye umuhimu mkubwa wa kijeshi, kwenye mpaka na Uganda
Shambulizi la M23, ambalo operesheni zake kuu zilifanyika 2012 na 2013 na kukamata baadhi ya maeneo ya mashariki ya Congo, limeongeza mvutano uliokuwepo kati ya DRC na Rwanda.
DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwasaidia M23, ikiwemo kutuma majeshi kuvuka mpaka. Rwanda inakanusha tuhuma hizo. Uamuzi wa kuunda kikosi cha pamoja cha Umoja wa Afrika haujawekwa bayana iwapo utaihusisha Rwanda.