Zaidi ya hatimiliki elfu moja ziko katika mchakato wa kubatilishwa, nyingine zikiwa za wanasiasa maarufu katika maeneo hayo. Serikali ya Kenya tayari imetangaza kuwa imekamilisha utaratibu unaohitajika kuwaondoa watu zaidi ya elfu kumi kutoka msitu huo wa Mau.
Kuondolewa kwa watu katika msitu wa Mau kumeibua hisia chungu nzima miongoni mwa wanasiasa, ambao wengine huchukulia ni mtaji wa kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuzungumza lugha inayowiana na raia wanaoathiriwa na kuondolewa kwa wakazi hao. Inaarifiwa kuwa wanasiasa wengi walijinyakulia vipande vya ardhi katika msitu huo miaka ya nyuma na kuwauzia wananachi ambao sasa wanatakiwa kuondoka katika msitu huo.
Waziri wa Mazingira
Waziri wa Mazingira wa Kenya, Keriako Tobiko, amesema kuwa hatimiliki zaidi ya 1,200 zimeorodheshwa kubatilishwa, akiongeza kuwa awamu hii ya pili haitamwacha yeyote aliyebadili msitu huo kuwa makazi yake.
“Msitu wa Maasai Mau ni sharti urejeshwe, si suala la majadiliano. Urejeshwe sasa au tusahau. Hamna jawabu jingine. Msitu huo wa Mau una umuhimu mkubwa mno si tu kwa jimbo pekee au vizazi vya sasa lakini pia vizazi vijavyo,” amesisitiza Waziri.
Hata hivyo, hapakosi mvutano wa aina yake, kati ya serikali na wakazi wa Msitu wa Mau, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiilaumu serikali ya Kenya kwa kutolifuatilia suala hilo kwa utaratibu unaofaa.
Wanasiasa washutumiwa
Lakini serikali ya Kenya mara kwa mara imeeleza kuwa haina haja ya kuwafidia watu waliopora ardhi ya serikali, kwa kujinyakulia vipande vya ekari nyingi na kubadili msitu huo na kuwa makazi yao. Waziri Tobiko amewashutumu wanasiasa kwa kuwatumia wananchi kujinufaisha.
Waziri ameeleza kuwa mgogoro ambao umekuwapo umekuwa wa kisiasa; sisi si wanasiasa. Sina nia ya kuwa mwanasiasa. Mau si msitu wa jamii fulani. Sitambui kabila unalotoka.
Katika awamu ya pili iliokamilika Julai, serikali imerejesha zaidi ya ekari elfu kumi na mbili za msitu huo na watu zaidi ya elfu kumi kuondolewa na majengo yao kubomolewa katika ardhi ya msitu huo wa ekari 46,000 eneo la Narok. Serikali ya Kenya imeeleza kuwa ina mpango mpana wa kuuhifadhi na kuutunza msitu huo ambao ni chemchem ya maji kwa maelfu ya raia wa Kenya.
Matokeo ya jopo la usuluhishi
Awali pameundwa jopo kazi la kutafuta suluhu ya kutunza msitu huo na ikibainika kuwa sababu za kuharibika kwa msitu huo ni kupitia unyakuzi wa vipande vya ardhi na watu wanaobadili maeneo hayo kuwa makazi yao, ukataji na uchomaji wa miti kiholela na vile harakati za jamii za wafugaji kutafuta chakula cha mifugo yao.
Mbunge wa Narok Kaskazini, Kenya, Moitalel Ole Kenta anaeleza kuwa ni jambo zuri kwa serikali kuutunza msituo huo ambao unawafaidi wakenya wengi kama chanzo cha maji.
Raila Odinga
Mwaka wa 2013, kulitokea ufurushaji wa watu katika msitu wa Mau, operesheni iliyoendeshwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Operesheni hiyo ilizuwa mgogoro wa kisiasa huku viongozi wa jamii zilizopinga harakati za kufurushwa wakiongozwa na William Ruto, ambaye sasa ni Naibu Rais wa Kenya, zikimshtumu kwa mwenendo usiofaa.
Hata hivyo, Odinga wakati huo aliahidi kuuendeleza mchakato huo hata kama utamuondolea umaarufu wa kisiasa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya