Senegal yasimamisha kwa muda uchimbaji madini kwenye mpaka wake na Mali

Ramani ya Senegal

Senegal ilisema Jumanne kwamba imesimamisha kwa muda shughuli za uchimbaji madini kwenye ukingo wa mto ambao ni sehemu ya mpaka wake wa kusini mashariki na Mali, kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kulinda afya ya wenyeji.

Mto Faleme, ukingo mkuu wa Mto Senegal, unakabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira na matumizi makubwa ya kemikali katika migodi ya dhahabu ambayo imekuwa mingi katika eneo hilo.

“Hali hii inayotia wasiwasi inahitaji hatua madhubuti kwa upande wa mamlaka za kitaifa kutafuta suluhu la haki kwa malalamiko yasiyoisha kutoka kwa watu wanaoishi kando ya mto”, wizara ya madini ilisema katika ripoti wiki iliyopita.

Kusimamishwa kwa shughuli hizo kwa miaka mitatu, hatua ambayo itatekelezwa hadi tarehe 30 Juni, mwaka 2027, inahusu eneo la mita 500, kando ya ukingo wa kushoto wa mto Faleme, kulingana na amri ya rais iliyochapishwa Jumanne.