Serikali ya Marekani imetoa salamu za pongezi za mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa Waislam wote ulimwenguni.
Katika tamko lake lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema “Kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mimi na Renda kwa dhati kabisa tunapenda kuwatakia Waislam wote ulimwenguni mfungo mwema wa Ramadan wenye amani na baraka nyingi.
Tillerson amesema mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa ibada, ukarimu na mazingatio.
Ameongeza kuwa aidha ni wakati wa kuwa karibu na familia na marafiki na kutoa sadaka kwa wale ambao wanaishi katika mazingira magumu.
“Wakati huu unatukumbusha mambo ya msingi ya kimaadili ya kushikamana na kuhurumiana ambayo sote tunayathamini,” amesema Tillerson.
“Nawatakia wote wanaofunga Ramadhan Kareem,” amesema.