Rwanda 'inazingatia' uamuzi wa serikali mpya ya Uingereza kuvunja makubaliano ya uhamiaji

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer, akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari, mjini London, Julai 6, 2024.

Rwanda Jumatatu ilisema “inazingatia” uamuzi wa serikali mpya ya chama cha Labour nchini Uingereza kufuta makubaliano yenye utata ya kuwafukuza wahamiaji wanaotafuta hifadhi nchini humo na kuwahamishia katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Waziri mkuu Keir Starmer alitangaza siku ya Jumamosi kwamba mpango wa uhamiaji wa serikali inayoondoka madarakani ya chama cha Conservative, “umekufa na kuzikwa.”

Tayari mpango huo ulikuwa umekabiliwa na changamoto kadhaa za kisheria, huku Mahakama ya Juu ya Uingereza ikisema katika uamuzi wake wa mwezi Novemba mwaka jana kwamba ulikuwa unakiuka sheria za kimataifa.

“Rwanda inazingatia nia ya serikali ya Uingereza kusitisha mkataba wa ushirikiano wa uhamiaji na maendeleo ya kiuchumi, kama ilivyoelezwa chini ya masharti ya mkataba uliopitishwa na mabaraza yetu mawili ya bunge,” ofisi ya msemaji wa serikali Yolande Makolo ilisema katika taarifa.

“Rwanda imetekeleza kikamilifu wajibu wake katika makubaliano hayo, ikiwemo kuhusu fedha, na bado ina dhamira ya kutafuta suluhu kwa mzozo wa kimataifa wa wahamiaji, ikiwemo kutoa usalama, utu na fursa kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokuja nchini kwetu,” taarifa hiyo iliongeza.

Chama cha Labour kilisema kabla ya uchaguzi wa Julai 4 kwamba kitafutilia mbali mpango huo, ambao serikali ya Conservative iliuzindua kuzuia idadi kubwa ya wahamiaji wanaojaribu kuingia Uingereza kupitia njia haramu kwa kutumia boti kutoka kaskazini mwa Ufaransa.

Mapema mwaka huu, waziri mkuu wa zamani Rishi Sunak aliongeza juhudi kupitisha sheria bungeni inayothibitisha kuwa Rwanda ni nchi salama, kuruhusu safari za ndege za wahamiaji kuendelea licha ya wasiwasi kuhusu sheria za haki za binadamu.