Rio 2016: Medali zaanza kubebwa katika siku ya kwanza

Bondia wa Cameroon Simplice Fotsala, kushoto, akipambana na Mwingereza Galal Yafai katika michuano ya awali ya ndondi.

Michezo ya Olimpiki ya Rio yaliingia katika siku ya kwanza kamili ya mashindano kwa michuano ya ndondi, volleyball, uogeleaji na mashindano ya baiskeli. Matukio makubwa ni pamoja na mechi ya mpira baina ya timu za wanawake za Marekani na Ufaransa, wakati katika basketball Marekani inapambana na China.

Ufunguzi wa 2016 Rio Olympics

​Kijana wa Kimarekani anayeshindana katika kulenga shabaha Ginny Thrasher alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujinyakulia medali ya dhahabu kwa kuwashinda washindani wake kutoka China katika raundi za fainali.

Mashindano Jumamosi yalifuatia sherehe za ufunguzi zilizojaa mbwembwe za utamaduni wa Brazil na hata changamoto zake za kijamii na kiuchumi.

Rais wa mpito wa Brazil Michel Temer alihudhuria ufunguzi huo katika uwanja mkuu wa Maracana huku viongozi kadhaa wa dunia nao wakiwa miongoni mwa wageni wa heshima.

Mwanariadha mkongwe na maarufu duniani Kipchego Keino wa Kenya alitunukiwa tuzo la kwanza Olimpiki lililobuniwa na kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC) kwa mchango wake katika michezo ya Olimpiki na jamii kwa jumla.