Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 02, 2025 Local time: 23:52

Kip Keino wa Kenya apata tuzo maalum la Olimpiki


Kipchoge Keino
Kipchoge Keino

Na BMJ Muriithi

Mwanariadha mkongwe na bingwa wa mara mbili wa Olimpiki, Kipchoge Keino, siku ya Ijumaa alipata tuzo maalum na la kipekee, wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya mwaka huu ya Olimpiki, uliofanyika mjini Rio De Jeneiro, Brazil.

Keino, mwenye umri wa miaka 76 na ambaye ni raia wa Kenya, alikabidhiwa tuzo hilo liitwalo Olympic Laurel Award, lililobuniwa na kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC).

'Kip' aliingia katika historia kama mwanariadha wa kwanza ulimwenguni kupokea kombe hilo lililotengenezwa kwa jiwe kutoka mji wa zamani wa Olimpia, na ambalo linakusudiwa kutambua mchango mkubwa wa wanariadha katika kuinua maisha ya jamii zenye mahitaji.

Keino, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa kamati ya Olimpiki nchini Kenya, amewahi kushinda dhahabu mara mbili katika Olimpiki, ikiwa ni mwaka wa 1968 na 1973. Mwanariadha huyo pia ameweka rekodi kwa kushinda dhahabu mara tatu katika mashindano ya jumuiya ya madola.

Kabla ya kukabidhiwa kombe hilo mbele ya maelfu ya mashabiki waliohudhuria sherehe za mwaka huu, Keino alishangiliwa alipoingia uwanjani humo akikimbia huku akiandamana na wanariadha wa kizazi kipya. Baadaye video fupi iliyoonyesha maisha ya mwanariadha huyo ilichezwa.

"IOC imeamua kuwatuza watu ambao wanachangia elimu, utamaduni, maendeleo na amani kupitia michezo," alisema mwenyekiti wa IOC, Thomas Bach, kabla ya kumpokeza Bwana Keino kombe hilo.

Bach alisema kuwa majaji wote ambao wanawakilisha bara zote za dunia, walikubaliana kwa kauli moja kwamba Keino ndiye alifaa kuwa mtu wa kwanza kupata tuzo hilo.

Mnamo mwaka wa 1973, baada ya kustaafu kutoka mashindano ya riadha, Keino alianzisha makao ya watoto yatima mjini Eldoret nchini Kenya, ambayo sasa ni hifadhi ya takriban watoto mia moja. Aidha, alianzisha shule iliyopewa jina lake mnamo mwaka wa 1999, ambayo hutoa mafunzao kwa tvijana wapatao mia tatu kila mwaka.

Keino pia ameanzisha kituo cha mazoezi na cha kutoa mafunzo kwa wanariadha chipukizi wanaoonyesha ari ya kwendelea na mashindano ya kimataifa.

Akipokea tuzo hilo Ijumaa, Keino alielezea furaha yake na kutoa wito kwa wanariadha na wanaspoti kwa jumla kujiunga naye na kuwasaidia vijana walio na mahitaji kupata chakula, makaazi na elimu.

"Tulikuja duniani bila chochote na tutaondoka bila chochote," alisema Kip Keino, huku akishangiliwa.

Kombe hilo litapewa mwanariadha mmoja katika ufunguzi rasmi wa mashindao ya wakati wa kiangazi ya Olimpiki kila baada ya miaka minne.

Mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu yataendelea kwa muda wa siku 16 hadi tarehe 21 mwezi Agosti mwaka huu.

XS
SM
MD
LG