Kiongozi wa chama tawala cha ANC Cyril Ramaphosa ameapishwa Alhamisi kuwa rais wa Afrika Kusini kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa rais Jacob Zuma.
Chini ya saa 24 baada ya Jacob Zuma kujiuzulu usiku wa jana, hivi sasa Africa Kusini imepata rais mpya: Cyril Ramaphosa, mfanyabiashara na mkereketwa wa chama cha ANC, ambaye alikuwa mstari wa mbele kumshinikiza Zuma kujiuzulu.
Ramaphosa aliteuliwa katika bunge bila ya upinzani Alhamisi mjini Cape Town, na kuapishwa muda mfupi baadae.
Tukio hilo limekuja baada ya saa 12 baada ya Zuma kukubaliana na shinikizo la chama chake kuachia madaraka kabla ya muhula wake kumalizika kati kati ya mwaka 2019.
Ramaphosa, ambaye ametumikia miaka minne iliyopita katika nafasi ya makamu wa rais chini ya Zuma na kuchukua uongozi hivi karibuni kutoka kwake kama rais wa ANC, amewaahidi wabunge atafanya jitihada ya kuliunganisha taifa.