Kiongozi huyo wa mrengo mkali wa kulia alipokea almasi hizo kutoka Saudi Arabia, kulingana na chanzo ambacho kina taarifa kuhusu tuhuma hizo.
Chanzo cha pili kimethibitisha mashtaka hayo, ingawa hakikueleza ni kuhusu makosa gani. Maafisa wote wawili walizungumza kwa mashtari ya kutotajwa majina.
Mahakama ya juu ya Brazil bado haijapokea ripoti ya polisi pamoja na mashtaka hayo. Itakapopokea ripoti hiyo, mwendesha mashtaka mkuu, Paulo Gonet, atakagua hati hiyo na kuamua kama atafungua mashtaka na kumlazimisha Bolsonaro kujitetea katika kesi dhidi yake.
Mashtaka hayo yameibua hisia kubwa katika msururu wa uchunguzi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani mwenye utata, yamepongezwa na wapinzani wake lakini yakalaaniwa na wafuasi wake wakisema ni unyanyasaji wa kisiasa.
Bolsonaro na mawakili wake walikanusha makosa yoyote kuhusiana na kesi hiyo, vile vile na msururu wa uchunguzi unaomkabili rais huyo wa zamani.