Rais Mpya wa Somalia Ajipanga Kutatua Matatizo ya Usalama, Ufisadi

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo

Rais Mpya wa Somalia ameapishwa rasmi Jumatano, katika sherehe zilizoandaliwa Mogadishu na kuahidi kuanza mara moja kuimarisha nchi hiyo iliyo sambaratishwa na vita, lakini akiwakumbusha wananchi kazi hiyo itachukua miaka mingi.

Mohamed Abdullahi Mohamed, ambaye ni maarufu kwa jina la “Farmajo” ameapa kuchukua wadhifa huo mjini Mogadishu akishuhudiwa na marais wa mataifa matatu jirani na dazeni za wanadiplomasia, akiwemo balozi wa Marekani nchini Somalia, Stephen Schwartz.

Farmajo amewaomba Wasomali kumsaidia kuleta utulivu nchini kwani nchi hiyo imepita katika miongo kadhaa ya misukosuko ya kivita iliyochochewa na ushindani wa kiukoo na wapiganaji wa Kiislamu, na ukame ambao umefanya hali ya nchi hiyo iwe mbaya zaidi.

“Matatizo ambayo Somalia inapitia imekuwa ni malimbikizo ya migogoro ya zaidi ya miaka 20 na ili kutatua matatizo yote haya inaweza kuchukua zaidi ya miaka 20 mingine,” amesema.

“Ninapenda kutatua matatizo haya katika kipindi cha miaka minne ijayo nikiwa madarakani lakini sirahisi.”

“Naomba mnisaidie kukabiliana na mambo muhimu na masuala makubwa, likiwemo suala la usalama, ukame, utawala wa sheria, utekelezaji wa haki na kutafuta suluhu, ambayo nafikiri serikali yangu inaweza kutatua haya katika kipindi cha miaka minne,” rais amesema.

Mara baada ya rais kuzungumza, Uingereza iliahidi dola za Marekani milioni 125 ikiwa ni msaada ambao utasaidia kununua chakula cha dharura kwa watu milioni moja wa Somalia.

Rais Farmajo ameahidi kupambana na ufisadi, baada ya uchaguzi wa urais kutokana na baadhi ya wagombea kudai kuwa wamelipa mamilioni ya dola kwa wabunge ikiwa ni katika mbinu zao za kupata kura.

“Nitarudisha imani kati ya serikali na wananchi wake, na niliahidi kwa Wasomali na ulimwengu kwamba serikali yangu itajaribu kubadilisha uelewa hasi wa dunia kwamba Somalia ni taifa lenye ufisadi,” rais huyu mpya amesema.

Sherehe hizo zilifanyika Jumatano katika viwanja vya uwanja wa ndege wa kimataifa Mogadishu, kama vile ilivyokuwa wakati wa uchaguzi; uwanja ambao unalindwa na majeshi ya Umoja wa Afrika.

Lakini kinyume na wakati wa uchaguzi, sherehe za kuapishwa ziliwajumuisha wasanii wa Somalia, waimbaji na wanamuziki, ambao walieleza matumaini yao juu ya kupatikana amani Somalia.