Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 27, 2024 Local time: 03:28

Wakenya Wengi Hawawezi Kufikia Tiba ya Saratani


Teknolojia ya kutibu maradhi ya saratani bado ni gharama kubwa kwa nchi kama Kenya.
Teknolojia ya kutibu maradhi ya saratani bado ni gharama kubwa kwa nchi kama Kenya.

Saratani au kansa ni moja ya magonjwa yanayochangia vifo kote ulimwenguni huku takwimu mpya za shirika la afya duniani, WHO, zikionyesha kuwa kila mwaka watu milioni 8.8 wanakufa kutokana na saratani, wengi wao katika mataifa yanayoendelea.

Katika taarifa yake mapema mwezi huu mkurugenzi wa shirika la afya duniani katika idara ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ambukiza, Dkt Etienne Krug, amesema kuwa moja ya tatizo la ugonjwa huu ni kuchelewa kutambuliwa kwake.

Lakini ameongeza kuwa tatizo hili sio tu linazikabili nchi zinazoendelea bali lipo pia katika mataifa ambayo yanavyo vifaa bora vya matibabu vya kisasa.

Saratani ni aina za magonjwa yanayoanzishwa na seli za mwili zinazoanza kujigawa ama kukua bila utaratibu wa kimaumbile.

Saratani ya Damu yaongoza

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA katika makala ya afya wiki hii ameangalia saratani za damu. Ameanza kwa kuelezea kuwa saratani za damu ni kati ya saratani zinazoathiri watu wengi, huku takwimu huko Uingereza zikionyesha kuwa kwa kila dakika 20 mtu mmoja anagunduliwa kuwa na saratani ya damu, ikiwa ni sawa na watu 70 kwa siku na watu 25,000 kwa mwaka.

Chanzo cha Saratani ya Damu

Daktari wa saratani hapa Mombasa katika hospitali za Agakhan, Riaz Kasman ameeleza kuwa kama ilivyo kwa aina mbali mbali za saratani, chanzo cha saratani ya damu hakiko wazi kama vile ilivyo rahisi kugundua ugonjwa wa malaria. Lakini madaktari wanahusisha sana na miale ya mabomu wakati wa vita na mitindo ya kimaisha.

Anazidi kufafanua kuwa “Multiple Myloma” ambayo ni moja ya saratani za damu ambayo inaambatana na maumivu makali ya mifupa kufuatia kuathirika kwa “bone marrow” au aina ya ute ulioko ndani ya mifupa kwa mtu muathirika. Hii ni kati ya sartani zinazosumbua wakenya.

Akiwa anaendesha gari lake ni nadra kwa mtu kufahamu kinachomsumbua mchungaji Paul Selel wa kanisa la kisima cha Neema kusini mwa pwani ya Kenya. Selel ni kiongozi wa kanisa na baba wa watoto wawili.

Namna ya kuitambua saratani

Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa Selel amekuwa akitibiwa saratani, lakini swali la msingi ni vipi alifahamu analo tatizo hilo?

Mwandishi wa VOA amesema Kasisi Selel ameeleza kuwa ilibidi alazwe hospitali baada ya tatizo lake hilo kufikia kipindi cha yeye kushindwwa kutembea na hivyo kulazimika kutumia kiti cha magurudumu.

Selel anasimulia kuwa akiwa mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa na Dkt Kasman alimuuliza tabibu huyu kuhusu tiba ya saratani hii ambayo pia inavunja hata mifupa.

Akiwa amerejea katika shughuli zake japo sio kwa kasi kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma, selel alipitia matibabu ya “chemotherapy” kwa kutumia dozi 29 na hata wakati mwengine alilazimika kutumia mara mbili kwa wiki, hali ambayo ilimfanya kuwa mchovu kutokana na nguvu ya madawa ambayo mgonjwa anatakiwa kunywa.

Tiba ya Saratani bado ni Ghali Kenya

Tiba ya saratani nchini Kenya ni ghali mno, ambapo Selel anaeleza namna ugonjwa huo unavyotia umaskini, kwani mgonjwa huuza kila alichonacho katika jitihada ya kutafuta tiba.

Kauli ya Selel inathibitisha umuhimu wa mgonjwa kuweza kuiwahi saratani kabla haijaenea mwili mzima. Kadhalika Dkt Kasman anasistiza kuwa ni sharti kwa watu kufika hospitalini mara tu wanapojitambua kwamba wana dalili za saratani huku akihimiza watu wabadili mitindo yao ya maisha na vyakula.

Daktari huyo anasema kuwa gharama za matibabu ya saratani imeendelea kuwa ghali kiasi cha kwamba Wakenya waliowengi wanapoteza maisha na kudhoofika kwa sababu ya kukosa matibabu. Pia maradhi hayo yamepelekea wengi kufilisika kwa kutumia mali zao kutafuta tiba huku wengine wakitafuta wahisani ili waweze kupata matibabu.

Ukosefu wa wataalamu wachangia

Lakini kwa upande wa mwengine wataalamu wanakerwa na ukosefu wa madaktari katika zahanati za umma ambao wana uwezo wa kutambua dalili za kwanza za saratani na kuitaka serikali kuekeza katika matibabu ya saratani kama wanavyofanya kwa maradhi mengine kama malaria, kifua kikuu na virusi vya ukimwi.

Hata hivyo wagonjwa wa saratani huenda wakapata afueni endapo bunge la Kenya litajadili na kuidhinisha msuada wa kurekebisha sheria ya kuzuia na kutibu saratani wa mwaka 2016, ulioletwa na mbunge wa kaunti ya Homabay, Gladys Wanga, utakao hakikisha kuwa saratani inajumuishwa katika tiba za afya ya msingi.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Amina Chombo, Kenya.

XS
SM
MD
LG